Mazingira FM

NHIF Mara kusajili kaya 21,273 awamu ya pili bima ya afya kwa wote

23 October 2026, 3:45 am

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi akimkabidhi kadi ya bima ya afya

Kaya 9,613 zenye wanufaika 25,790 ndizo zilizofanikiwa kusajiliwa bima ya afya awamu ya kwanza, hali ambayo inaonesha kuwa usajili haukufikia lengo la chini la kitaifa la asilimia 65.

Na Adelinus Banenwa

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi, amesema Mkoa wa Mara haukufikia kiwango kilichotarajiwa katika awamu ya kwanza ya usajili wa wananchi kwenye mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, baada ya kusajili asilimia 41 ya kaya zilizolengwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa usajili wa wananchi katika Bima ya Afya kwa Wote, uliofanyika katika viwanja vya Mkendo, mjini Musoma, Mtambi amesema awamu ya kwanza ililenga kusajili kaya 14,148 zenye jumla ya wanufaika 62,256.

Hata hivyo, kaya 9,613 zenye wanufaika 25,790 ndizo zilizofanikiwa kusajiliwa, hali ambayo inaonesha kuwa usajili haukufikia lengo la chini la kitaifa la asilimia 65.

Baadhi ya wananchi kwenye banda la NHIF wakipata ufafanuzi wa Bima ya afya kwa wote

Mtambi amesema huenda matokeo hayo yalisababishwa na wananchi kutopata taarifa za kutosha kuhusu mpango huo au kuwepo kwa uhamasishaji usiotosheleza, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za kutoa elimu na kuhamasisha jamii ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma za bima ya afya.

Ameeleza kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha mpango huo na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kupitia bima.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi

Awali, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mara, Kuhunga Patric Msambichaka, alisema awamu ya pili ya usajili inalenga kufikia kaya 21,273 zenye jumla ya wanufaika 44,786.

Msambichaka alisema kuwa lengo hilo linahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali pamoja na uhamasishaji wa kutosha ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na kujiunga na mpango huo.

Sauti ya Kuhunga Patric Msambichaka

Uzinduzi wa awamu ya pili unakuja huku Mkoa wa Mara ukiwa na jukumu la kuongeza mwitikio wa wananchi katika usajili wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kufikia malengo yaliyowekwa na kupanua fursa za wananchi kupata huduma za afya kupitia mfumo wa bima.