Mazingira FM
Mazingira FM
4 November 2026, 2:24 pm

DC anasema taarifa za mipango inayofanyika kwa siri ya kuwakeketa watoto zinafahamika kupitia vyombo vya kiintelijensia, huku akibainisha kuwa watakaobainika wanakabiliwa na faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano hadi 15.
Na Adelinus Banenwa
Onyo kali limetolewa kwa wazazi na walezi wanaopanga kuwakeketa watoto wa kike, huku serikali ikisisitiza kuwa haitamvumilia wala kumsamehe mtu yeyote atakayebainika kushiriki katika vitendo hivyo vinavyohatarisha maisha na haki za watoto.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, katika mikutano ya kutoa elimu dhidi ya ukeketaji iliyofanyika Kata za Machochwe na Mbalibali, ambapo amesema serikali ina wajibu wa kuwalinda watoto, ikiwemo kuwahifadhi katika nyumba salama ili waendelee na masomo na kutimiza ndoto zao. Ameeleza kuwa taarifa za mipango inayofanyika kwa siri ya kuwakeketa watoto zinafahamika kupitia vyombo vya kiintelijensia, huku akibainisha kuwa watakaobainika wanakabiliwa na faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano hadi 15.
Aidha, Angelina amewaonya viongozi wa mitaa, madiwani na polisi wa kata kutowakingia kifua wahusika wala kuingilia utekelezaji wa sheria kwa kuwaombea msamaha. Pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ufuatiliaji ili kubaini wazazi na ngariba wanaopanga kutekeleza ukeketaji, hususan wanaoratibu tarehe za kufanya vitendo hivyo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly, ameeleza madhara ya ukeketaji, ikiwemo vifo vinavyotokana na kuvuja damu nyingi pamoja na mila zilizokuwa zikihusisha kutupa miili ya waathirika porini. Amewataka wazee wa mila kushiriki katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo badala ya kuviratibu au kuvichochea, akibainisha kuwa ukeketaji unasababisha watoto wa kike kukatiza masomo na kuingia katika ndoa za utotoni.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wameitaka serikali kuongeza juhudi za kukomesha ukeketaji, wakieleza kuwa watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo wakati mwingine huanza kupewa hadhi na majukumu ya watu wazima kwa kuaminika kuwa tayari wamekomaa na si watoto tena, hali inayochangia kuhusishwa na vibuli badala ya kuendelea kupata malezi na ulinzi unaostahili.