Storm FM

Kikundi cha NEPA Nyarugusu chatoa vifaa tiba, zawadi kwa wagonjwa

17 December 2025, 9:18 pm

Moja ya ujumbe kutoka Kikundi cha NEPA wakati kikiwa katika kituo cha afya Nyarugusu kutoa zawadi kwa wagonjwa na vifaa tiba. Picha na Mrisho Sadick

Kikundi hicho kabla ya kufanya mkutano mkuu wa mwaka , kimefanya matembezi kuelekea katika kituo cha afya Nyarugusu kwa ajili kutoa zawadi kwa wagonjwa , vifaa tiba pamoja na kuchangia damu.

Na Mrisho Sadick:

Viongozi wa dini katika Kata ya Nyarugusu wilayani Geita wamekipongeza kikundi cha kijamii cha NEPA kwa mchango wake mkubwa wa kugusa maisha ya wananchi, baada ya kikundi hicho kutoa msaada wa vifaa tiba pamoja na kuwasaidia wagonjwa katika Kituo cha Afya Nyarugusu.

Viongozi wa dini wamesema kitendo kilichofanywa na kikundi cha NEPA ni cha kizalendo na chenye kugusa mioyo ya wananchi, hasa ikizingatiwa changamoto za upatikanaji wa huduma za afya katika baadhi ya  maeneo ya vijijini kuwa changamoto huku wakivitaka vikundi vingine vya kijamii, taasisi binafsi pamoja na wadau wa maendeleo kuiga mfano huo kwa kushirikiana na Serikali.

Kikundi cha NEPA kikiwa katika matembezi maalumu kuelekea katika kituo cha afya Nyarugusu. Picha na Mrisho Sadick

Mwenyekiti wa kikundi cha NEPA Morris Julius amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kusaidiana wakati wa changamoto na misiba mbalimbali, lakini pia kuamua kupanua wigo wa msaada kwa kuigusa jamii inayowazunguka kwa kuwasaidia wahitaji. 

Meneja wa kampuni ya MESE MLELA’S ONE, ambaye ni mdau wa maendeleo anayeshirikiana na kikundi cha NEPA, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na kikundi hicho katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo sekta ya afya na elimu. 

Kikundi cha NEPA kikiwa katika kituo cha afya Nyarugusu kikitoa zawadi na vifaa tiba kwa uongozi wa kituo hicho. Picha na Mrisho Sadick

Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Lusekelo Mwaikenda, amesema Kituo cha Afya Nyarugusu kinahudumia kata tano ambazo ni Bukoli, Nyalwanzaja, Nyaruyeye, Lwamgasa pamoja na Nyarugusu nakwamba msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizopo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Sauti ya Ripoti hii na Mrisho Sadick