Wajasiriamali wa soko la Lukilini kujengewa vizimba 50
13 April 2024, 3:12 pm
Wafanyabiashara walio wengi hasa wale walioko katika maeneo ya vijijini au nje ya miji hukabiliwa na changamoto ya miundombinu duni ya kufanyia biashara zao
Na Kale Chongela – Geita
Baadhi ya wajasiriamali waliopo soko la Lukilini Mtaa wa Mkoani Kata ya kalangalala Mjini Geita wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mhe Costantine Kanyasu kwa kutoa fedha ili kuwejengea vizimba katika soko hilo.
Wakizungumza na Storm Fm wajasiriamali hao wamesema kuwa kukamilika kwa vizimba hivyo itawasadia baadhi yao kuachana na kuuzia chini na kwamba soko hilo litakuwa na mvuto katika biashara zao tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa mkoani ambapo ndipo soko la Lukilini lilipo Bw Salvatory Daniely amesema yupo tayari kusimamia fedha hizo ili zitumike kwenye malengo ambayo yamekusudiwa na si vitu vingine ili eneo hilo liweze kuwanufaisha wajasiriamli waliopo katika soko la lukilini .
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Tawi la CCM Mtaa wa Mkoani Bw Amos Daudi amesema kuwa jumla ya Fedha ambazo zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mhe Costantine John Kanyasu ni Milioni 30 kwa ajili ya kutengeneza vizimba 50 kwa ajili ya kupanga bidhaa katika soko hilo.