Storm FM

Mbunge Chato Kusini atoa bati 200 kuezeka jengo la shule

23 January 2026, 11:23 am

Viongozi mbalimbali wa kijiji, chama na shule ya msingi Ndalichako baada ya kukabidhiwa bati. Picha na Ester Mabula

Shule ya msingi Ndalichako iliyopo katika kijiji na kata ya Bwanga, halmshauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita ina jumla ya wa wanafunzi 1045

Na: Ester Mabula

Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini Mhe. Paschal Lutandula ametoa bati 200 ili kuezeka jengo lenye vyumba vitatu katika shule ya msingi Ndalichako, iliyopo Kata ya Bwanga wilayani Chato mkoani Geita.

Akikabidhi bati hizo kwa niaba ya mbunge, Katibu wa Mbunge, Joseph James, amesema Mbunge Lutandula ataendela kugusa maeneo mbalimbali kama alivyoahidi ili kuweza kudumisha ushirikiano na wananchi ndani ya jimbo lake huku akisisitiza mabati hayo kutumika kwenye lengo lililokusudiwa.

Sauti ya Joseph James, katibu wa mbunge
Josep James (kati), Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Chato kusini akizungumza na wananchi pamoja na wanafunzi (hawapo pichani). Picha na Ester Mabula

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Felister Shadrack ameeleza kufurahishwa na msaada huo akisema kuwa utasaidia kukamilisha zoezi la kuezeka majengo ya shule na kuchangia kupunguza tatizo la upungufu wa madarasa, hali itakayoongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.

Sauti ya mwalimu mkuu, Felister Shadrack

Mwenyekiti wa kijiji cha Bwanga Fares Enelicko amesema msaada uliotolewa na mbunge utasaidia kuchochea ufanisi wa walimu kufundisha.

Sauti ya mwenyekiti wa kijiji cha Bwanga

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wazazi wenye wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wameshukuru kwa msaada huo wakieleza namna ulivyowahamasisha kuchanga shilingi elfu 10 kila kaya kwaajili ya kusaidia gharama za matengenezo.

Sauti ya wananchi
Uezekaji wa jengo lenye vyumba vitatu ukiendelea baada ya kupokea bati kutoka kwa Mbunge. Picha na Ester Mabula