Storm FM
Storm FM
15 January 2026, 4:06 pm

Hatua hiyo imekuja katika kipindi hiki ambacho muhula mpya wa masomo umeanza katika shule mbalimbali nchini, huku serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa elimu jumuishi kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Na Mrisho Sadick:
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita imetangaza kuanza msako wa kuwabaini na kuwachukulia hatua wazazi wanaowaficha watoto wao wenye ulemavu, hali inayowanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la Wazazi wa CCM Mkoa wa Geita kilichofanyika ofisi za CCM Mkoa wa Geita Magogo, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoani humo Lucas Mazinzi amesema kitendo cha kuwaficha watoto wenye ulemavu ni kinyume na maadili, sheria za nchi pamoja na sera ya elimu inayotambua haki sawa kwa kila mtoto.

Mazinzi ametoa maagizo kwa wajumbe wote wa Jumuiya ya Wazazi katika wilaya zote za mkoa wa Geita kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa ngazi za chini pamoja na jamii kwa ujumla ili kuwafichua wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu, hatua itakayosaidia watoto hao kuandikishwa na kuanza masomo kama ilivyo kwa watoto wengine.
Kwa upande wao, wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Geita wameahidi kutekeleza maagizo hayo kwa vitendo kwa kushuka hadi katika mitaa na vijiji, wakiwahamasisha wazazi kuachana na imani potofu zinazodhoofisha maendeleo ya watoto wenye ulemavu na kwamba jamii inapaswa kuelewa kuwa watoto wenye ulemavu wana uwezo wa kusoma, kuelimika na kuchangia katika maendeleo ya familia na taifa endapo watapewa fursa sawa.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila, amewataka viongozi wa chama hicho kuendelea kushirikiana kwa karibu na watendaji wa serikali katika kutatua changamoto za kijamii ikiwemo elimu, afya na ustawi wa watoto huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kuacha kutunishiana misuli na badala yake kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya wananchi, hususan makundi yenye uhitaji maalum kama watoto wenye ulemavu.
Kasendamila ameongeza kuwa CCM itaendelea kusimamia sera na mipango inayolenga kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na kuheshimiwa, huku akitoa wito kwa jamii nzima ya mkoa wa Geita kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu bora na jumuishi.