Storm FM
Storm FM
9 January 2026, 7:31 pm

Jumla ya watoto 154 wanalelewa katika kituo cha watoto yatima cha Moyo wa huruma ambacho kinafadhiliwa na kampuni ya Geita Gold Minning Limited.
Na: Ester Mabula
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuwajibika kwa jamii pamoja na kuendeleza ufadhili wa kituo cha kulea watoto yatima cha Moyo wa huruma kwa kukabidhi hundi ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya kugharamia shughuli za kituo hicho kwa mwaka 2026.
Hafla ya makabidhiano imefanyika leo Januari 09, 2026 katika ukumbi uliopo katika kituo hicho kilichopo eneo la Jimboni, halmashauri ya manispaa ya Geita ambapo Mkurugenzi mtendaji wa GGML Bw. Duan Campbell amesema uwepo wa GGML sio tu kwaajili ya uchimbaji wa dhahabu bali pia ni kuweza kuigusa Jamii.

Askofu wa Jimbo katoliki Geita Flavian Kasala ameikumbusha Jamii kuendelea kujiepusha na mambo yanayopelekea ongezeko la watoto wanaoishi mazingira magumu kwani wapo watoto wengine wanakosa msaada.

Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ameipongeza kampuni ya GGML kwa kuendelea kuikumbuka Jamii kupitia CSR sambamba na kuendelea kusaidia makundi mbalimbali kwenye Jamii.

Akizungumza mara baada ya hafla ya kukabidhi hundi, Mwakilishi wa GGML kutoka idara mahusiano Mussa Shunashu ameeleza kuwa hicho kilianza mwaka 2006 kikiwa na jumla ya watoto 12 sambamba na kueleza majukumu ya GGML kwa kituo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya watoto wanaolelewa hapo Priscus Donati ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita pamoja na Suzana Vyatoli ambaye ni mlezi wa watoto katika kituo hicho wametoa shukrani na pongezi kwa GGML kwa kuendelea kufadhili kituo hicho.
