Storm FM

Marufuku hospitali kuzuia miili Geita

19 December 2025, 12:16 pm

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Jafari Rajabu Seif akizungumza kwenye kikundi cha UVINYA. Picha na Mrisho Sadick

Serikali  imeshatoa maelekezo kwa mamlaka zote za afya nchini kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa ipasavyo bila kuwepo vikwazo

Na Mrisho Sadick:

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Jafari Rajabu Seif amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita kuhakikisha hospitali zote zilizopo mkoani humo hazizuii wananchi kuchukua miili ya wapendwa wao kwa kisingizio chochote kwani ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Seif ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na Umoja wa Kikundi cha Vijana wa Nyarugusu Jimbo la Busanda wilayani Geita amesisitiza kuwa Serikali  imeshatoa maelekezo kwa mamlaka zote za afya nchini kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa ipasavyo bila kuwepo vikwazo au ucheleweshaji wowote huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo hilo.

Wajumbe wa UVINYA wakiwa kwenye mkutano mkuu wa kikundi. Picha na Mrisho Sadick

Awali Katibu wa kikundi hicho Mathias Kato akiwasilisha taarifa kwa Naibu Waziri amesema licha ya mafanikio mbalimbali waliyoyapata ikiwemo kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukosefu wa ofisi ya kudumu na mitaji ya kuendeleza shughuli zao huku mwenyekiti wa kikundi hicho Michael Kajanja akisema miongoni mwa miradi mipya watakao uanzisha ni pamoja kukodisha mashine ya kushushia miili makaburini ikiwa ni sehemu ya huduma ya jamii.

Wajumbe wa UVINYA wakiwa kwenye mkutano mkuu wa kikundi. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wao baadhi ya vijana wa kikundi hicho Ester Mihayo na Zaituni Hussein wamesema wana imani kubwa kuwa kupitia umoja na mshikamano walioujenga wataweza kubadilisha maisha yao kiuchumi na kijamii sambamba na kuleta maendeleo chanya katika Kata ya Nyarugusu.

Sauti ya Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick