Storm FM

Mapambano ya ugonjwa wa sikoseli yaanza Geita

3 December 2025, 7:18 pm

Kaimu katibu tawala mkoa wa Geita akizindua mradi wa KETAN SCD Mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mradi huo utatekelezwa kwa miaka miwili, utatoa huduma ya upimaji, utoaji wa bima za Afya kwa watoto zaidi ya 300 ambao hawana uwezo wa kumudu matibabu.

Na Mrisho Sadick:

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa sikoseli nchini, huku takwimu za Wizara ya Afya zikionyesha kuwa watoto takribani  elfu14,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa huo.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Ugonjwa wa sekoseli Taifa Dkt Irene Mpoki kwenye uzinduzi wa mradi wa KETAN SCD PROJECT katika Mkoa wa Geita wenye lengo la kuwafikia watu zaidi ya Elfu 30,000 kwenye Halmashauri tatu za Geita DC , Geita Manispaa na Mbogwe.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa KETAN SCD Mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkurugenzi wa Taasisi ya TASIWA inayotekeleza mradi huo Pascazia Mazeze amesema wamelanga kuboresha maisha ya wagonjwa wa sikoseli nakwamba mradi huo utatekelezwa kwa miaka miwili, utatoa huduma ya upimaji, utoaji wa bima za Afya kwa watoto zaidi ya 300 ambao hawana uwezo wa kumudu matibabu sambamba na kuziwesha kiuchumi baadhi ya familia zenye watoto wenye Ugonjwa huo.

Viongozi na wadau mbalimbali wa afya wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi. Picha na Mrisho Sadick

Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt Yohan Kihaga ameahidi kwenda kushirikiana na taasisi hiyo kuhakikisha wanatekeleza mradi huo kwa ufanisi huku akiiomba wizara ya afya kusaidia kuweka mfumo wa utambuzi wa takwimu kwa wagonjwa wa sikoseli.

Kaimu Katibu tawala wa Mkoa wa Geita Dkt Elfas Msenya amepongeza hatua hiyo huku akitoa wito kwa taasisi hiyo kuhakikisha inatoa bima kwa watoto wote watakao bainika kuwa na ugonjwa wa sikoseli wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Sauti ya Ripoti hii na Mrisho Sadick