Storm FM
Storm FM
25 July 2025, 3:27 pm

Hadi sasa serikali imefanikiwa kufikia asilimia 90 ya watu wanaotambua hali yao ya maambukizi, asilimia 98 wapo kwenye tiba, na asilimia 98 wamefubaza virusi.
Na: Ester Mabula
Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) limetoa pongezi kwa serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na baraza hilo katika jitihada madhubuti za mapambano dhidi ya janga la UKIMWI.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2025 katika ukumbi wa GEDECO halmashauri ya Manispaa ya Geita, Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Leticia Mourice Kapela amesema licha ya mabadiliko ya sera za wafadhili katika utoaji wa misaada, bado kuna upatikanaji wa dawa za ARV kwa watu wenye maambukizi.
Ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaendelea kupima VVU ili kutammbua afya zao na kuzingatia matibu na miongozo pindi wanapobainika kuwa na VVU.

Akizungumza Afisa Mtendaji mkuu wa baraza hilo Deogratius Rutatwa ameiasa Jamii kuacha vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI huku akieleza kuwa vinachangia watu kushindwa kuzingatia matumizi ya dawa pindi wanapogundua hali zao.
Aidha Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) limeeleza kuwa linaendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuhakikisha tunajenga uwezo katika kuimarisha afya, kuhamasisha na kuelimisha watu kutumia huduma za VVU, kupiga vita unyanyapaa wa aina zote, na kuendelea kuimarisha uhusinao na wadau mbalimbali katika kuiwezesha serikali kufikia malego yake.
