Storm FM
Storm FM
24 July 2025, 11:34 am

‘Geita Youth Sports Tournament’ imehitimishwa kwa kuzisogeza karibu shule za sekondari 40 kutoka halmashauri ya Manispaa ya Geita kupitia michezo mbalimbali.
Na: Ester Mabula
Kampuni ya uchimbaji madini ya Geita Gold Minning Limited (GGML) kwa kushirikiana na halmashauri ya manispaa ta Geita imeanzisha mashindano ya ‘Geita Youth Sports Tournament’ kwa shule za sekondari, yakilenga kuibua vipaji, kuondoa mdondoko wa wanafunzi kitaaluma, kuhamasisha ushiriki wa wanafunzi katika michezo na kuimarisha mahusiano miongoni mwa shule za manispaa hiyo.

Katika fainali za kuhitimisha mashindano hayo kwenye viwanja vya shule ya sekondari Nyankumbu Girls yaliyoanza tangu Julai 14, na kuhitimishwa Julai 22, 2025, Afisa elimu sekondari wa manispaa ya Geita, Rashid Mhaya, amesema michezo ni sehemu ya mkakati wa kupunguza utoro mashuleni kwani tangu kuanza kwa juhudi kama hizi, idadi ya wanafunzi wanaoacha shule imepungua.
Akizungumza mkurugenzi wa manispaa ya Geita ameipongeza kampuni ya GGML kwa kuendelea kushirikiana na serikali ya manispaa hiyo katika nyanja mbalimbali za elimu, Afya, miundombinu nk
Meneja rasilimali watu wa GGML Charles Masubi amesema usawa katika elimu kwa kila mtoto ni muhimu bila kujali hali yake ya maisha na kwamba wataendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuendeleza vipaji kupitia michezo mashuleni kama njia mojawapo ya kujenga taifa lenye msingi imara wa elimu.

Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Abdallah Komba, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye fainali hizo, amepongeza mashindano hayo na kuomba yawe ya kudumu kila mwaka, akisisitiza kuwa michezo ni chombo cha kujenga nidhamu, kuibua vipaji na kuwaepusha vijana na vishawishi hatarishi mitaani.
Katika fainali hizo zilizokutanisha shule 40 ikiwa 30 za serikali na 10 za Binafsi, Kalangalala Sekondari imeibuka bingwa kwa wavulana kwa kuifunga Kasamwa 3-2, huku upande wa wasichana Nyankumbu Girls ikichapa Geita Girls mabao 3 – 0.