Storm FM
Storm FM
15 May 2025, 5:12 pm

Jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 1.228 kimetolewa kwa vikundi 100 vinavyojumuisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuweza kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali.
Na: Ester Mabula:
Hafla ya utoaji wa mikopo hiyo imefanyika leo Mei 15, 2025 katika ukumbi wa St. Aloysious mtaa wa Shilabela mjini Geita.
Awali, akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, mkuu wa idara ya maendeleo ya Jamii manispaa ya Geita Robert Jackson Sungura ametaja idadi ya vikundi ambavyo vimepatiwa mkopo huo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kutaja mchanganuo wa kiasi kilichotolewa kwa kila kundi.

Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa ya Geita Mhe. Costantine Morandi ameeleza kuwa kwa sasa halmashauri ya manispaa ya Geita imepiga hatua katika kiwango cha fedha kilichotolewa kutoka shilingi milioni 600 mwaka wa fedha uliopita hadi shilingi Bilioni 1.228 iliyotolewa leo.
Mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Abdallah Komba amesema fedha zilizotolewa zikalete tija kwa wanufaika ili kuweza kuzalisha makundi mengi zaidi ya watu watakaonufaika na mikopo hiyo, kwani dhamira ya serikali ni kufikia watu wengi zaidi.

Aidha Mhe. Komba ameelekeza shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira bora ya kuwanufaisha wananchi kupitia mikopo ya halmashauri inayotolewa kote nchini.
Baadhi ya wanaufaika wa mkopo huo wakizungumza kwa niaba wa wenzao Frank Bukela na Lucia Khalfan wametoa shukrani kwa Rais Samia kwa kupatiwa mikopo hiyo.
