Storm FM
Storm FM
26 April 2025, 2:05 pm

“Na tukikupa bendera hii maana yake wewe ndio unaturudisha nyuma kwenye suala la usafi na unatakiwa kubadilika” – Mkuu wa wilaya ya Geita
Na: Kale Chongela:
Serikali wilaya ya Geita imeadhimisha siku ya kumbukizi ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuzindua kampeni ya usafi wa mazingira iliyofanyika katika mtaa wa Shilabela kata ya Buhalahala halmashauri ya Manispaa ya Geita ili kuhakikisha kila eneo linakuwa safi.
Akizungumza na wananchi akiwa katika Mtaa wa Shilabela, mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba amesema zoezi hilo la usafi litaambatana na zawadi katika mitaa ambayo itafanya vizuri sambamba na hilo zipo bendera ambazo zitatolewa kwa maeneo ambayo yataongoza kwa uchafu.
Aidha mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bw. Fredrick Masalu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanafanya usafi ili kuepukana na magonjwa yatokanayo na uchafu huku Kaimu mstahiki meya ambaye ni diwani wa kata ya kalangalala Prudence Temba akiwasihi wananchi kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Safia Jongo amesema kutokana na Geita kupanda hadhi kuwa manispaa kuna haja ya kila maeneo kufanyiwa usafi ili kulingana na hadhi ya manispaa ya Geita.

Kampeni hiyo imepewa jina la ‘HYAGULAGA GEITA’ ikimaanisha ‘Fagia/Safisha Geita’