Storm FM
Storm FM
12 April 2025, 8:42 pm

Jamii imeendelea kunufaika na elimu ya usalama pamoja na kukabiliana na vitendo vya uhalifu inayoendelea kutolewa mkoani Geita.
Na: Ester Mabula:
Wananchi wa mtaa wa Nyantorotoro A kata ya Nyankumbu katika halmashauri ya manispaa ya Geita wametoa pongezi kwa Jeshi la polisi kwa kushirikiana na Mgodi wa GGML kupitia elimu wanayoitoa kwa wananchi juu ya kukabiliana na uhalifu.
Wakizungumza leo Aprili 12, 2025 mara baada ya kupata elimu wananachi wameeleza kuwa elimu hiyo itawasaidia katika kufichua vitendo vya ukatili vinavyoendelea kwenye Jamii.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyantorotoro A amesema elimu hiyo imekuwa bora kutolewa kwa wakati huu na kuliomba Jeshi la polisi kuendelea kuwafikia wananchi zaidi ili kuweza kusaidia kutokomeza uhalifu.
Mrakibu wa polisi kutoka kamisheni ya polisi Jamii makao makuu Ezekiel Kyogo ametoa rai kwa Jamii kuwekeza katika malezi ya watoto na kuwafundisha uzalendo ambao utasaidia kuilinda Tanzania na kuwa na kizazi chenye kujali pasipo kuchochea vitendo vya uhalifu na ukatili.

Elimu hii inatolewa kupitia program maalum iliyozinduliwa Aprili 04, 2025 mkoani Geita yenye lengo la kukabiliana na uhalifu iliyopewa jina la Community Policing Outreach ambayo imebeba kaulimbiu isemayo ‘POLISI JAMII, NI WAJIBU WETU SOTE’