

3 April 2025, 5:56 pm
Jeshi la Polisi mkoani Geita limeandaa mpango maalum wa kuendelea kutoa elimu kwa Jamii ili kuweza kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwemo ukatili.
Na: Paul William:
Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Asteria Lunyilija (60) mkazi wa kijiji cha Bulela, kata ya Bulela, halmashauri ya manispaa ya Geita mkoani Geita ameuawa kikatili kwa kukatwa na silaha aina ya panga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu ambao bado hawajajulikana.
Tukio hilo limetokea siku ya jumapili Marchi 30, 2025 katika kijiji hicho majira ya saa mbili usiku wakati familia ya marehemu ikiwa inapata chakula cha usiku.
Akielezea tukio hilo Happynes Edson Kiboko ambaye ni mke wa mtoto wa marehemu amesema walisikia mtu akifungua mlango kwa nguvu ambapo marehemu alipojaribu kushindana na mtu huyo ndipo alipoanza kushambuliwa
Mdogo wa marehemu aitwae Mektlida Masele ameeleza kuwa familia imepata pigo kwa kumpoteza dada yake kwani alikuwa msaada mkubwa kwenye familia
Wananchi na wakazi wa kijiji cha Bulela wameiomba serikali kupitia kwa Jeshi la polisi kuweza kuwachukulia hatua kali wahusika pindi watakapobainika
Viongozi wa kitongoji na kijiji cha Bulela wameeleza kuskitishwa na tukio hilo na kuiomba Jamii kuacha kufanya vitendo vya uhalifu
Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na baada ya kufanya uchunguzi wa mwili liliruhusu mwili wa marehemu kusitiriwa huku uchunguzi ukiendelea.