

22 February 2025, 11:56 am
Mashirika mbalimbali ya kiraia yameendelea kuisaidia serikali katika uboreshaji wa miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Shule ya msingi Ikulwa iliyopo kata ya Ihanamilo wilayani Geita yenye wanafunzi zaidi ya 1000 iliyokuwa na upungufu wa matundu 53 ya vyoo, Februari 20, 2025 imekabidhiwa matundu kumi na nane ya vyoo vilivyojengwa na mradi wa KAGIS unaotekelezwa shirika la Plan International ili kupunguza changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika shule hiyo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa matundu 18 ya vyoo pamoja na chumba cha hedhi salama, mwalimu mkuu wa shule hiyo Daniel Nzoka amesema awali shule hiyo ilikuwa na matundu manne ya vyoo kwa upande wa wavulana na matundu manne kwa upande wa wasichana.
Mkurugenzi mkazi wa mradi wa KAGIS Tanzania Jane Isambuche amesema shirika la Plan International kupitia mradi wa KAGIS kwa kushirikiana na serikali wametekeleza miradi ya ujenzi wa vyoo vya kisasa katika shule 9 zilizopo mkoani Geita.
Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Geita Bw. Herman Matemu ambaye ni Kaimu katibu tawala wa mipango na uwekezaji mkoa wa Geita ameupongeza mradi huo kwa kuiunga mkono serikali katika utekelezaji wa miradi ambayo inalenga kupunguza changamoto mbalimbali kwa baadhi ya shule mkoani Geita.