Storm FM

Wananchi Narusunguti washukuru kujengewa zahanati

17 February 2025, 3:26 pm

Jengo la zahanati ya kijiji cha Narusunguti ambalo limezinduliwa. Picha na Edga Rwenduru

Wananchi wa kijiji cha Narusunguti hatimaye waagana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika maeneo jirani.

Na: Edga Rwenduru – Geita

Wananchi wa kijiji cha Narusunguti kata ya Busonzo wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameishukuru serikali kwa kuwajengea zahanati katika kijiji hicho ambapo awali walikuwa wakiteseka kufuata huduma hiyo katika kata jirani ya Uyovu huku gharama za usafiri zikitajwa kuwa ni changamoto hasa nyakati za usiku.

Mradi huo wa zahanati umejengwa kwa msaada wa mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF kwa ushirikiano na wananchi wa kijiji cha Narusunguti.

Akikabidhi zahanati hiyo kwa niaba ya mganga mkuu wa wilaya ya Bukombe William Mayila ambaye ni Afisa afya wilayani Bukombe, amewasihi wananchi kuutunza mradi huo kwa manufaa ya jamii hiyo.

Sauti ya Afisa Afya William Mayila
Mwenyekiti wa kijiji cha Narusungi Kasema Mashauri Lukaga. Picha na Edga Rwenduru

Kasema Mashauri Lukaga ni mwenyekiti wa kijiji cha Narusunguti amesema jengo hilo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 103 mpaka kukamilika kwake huku akisema zahanati hiyo itaondoa adha hasa kwa kina mama wajawazito.

Sauti ya mwenyekiti Kasema Mashauri

Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo huku akina mama wakiomba kupewa ujauzito kutokana na uwepo wa zahanati hiyo

Sauti ya wananchi

Naye diwani wa kata ya Busonzo Mhe. Safari Mayala ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa zahanati hiyo ameipongeza serikali kwa kuondoa changamoto hiyo katika kijiji hicho.

Sauti ya Diwani Mayala
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Narusunguti kwenye uzinduzi wa zahanati. Picha na Edga Rwenduru