Storm FM

Wakazi Chibingo watoa eneo kwa ajili ya shule

8 September 2024, 3:41 pm

Wananchi wa kijiji cha Chibingo wakishiriki kusafisha eneo la ujenzi wa shule maalumu ya sekondari. Picha na Evance Mlyakado

Wakazi wa kijiji cha Chibingo, kata ya Nyamigota wilaya na mkoani Geita wamejitolea eneo lao kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari.

Wananchi wa kijiji cha Chibingo wamehamasika kushiriki katika usafi wa eneo hilo ambapo itajengwa shule itakayohusisha mafunzo ya ufundi, kilimo na michezo ili kuendana na sera ya elimu ijayo yenye lengo la kuwajengea wanafunzi watakaomaliza shule uwezo na ujuzi katika shughuli mbalimbali za ujasiliamali.

Akizungumzia ujenzi wa shule hiyo mpya afisa mtendaji wa kata ya Nyamigota ambapo kipo kijiji hicho Kazimili Malindi amesema ujenzi huo unatekelezwa kwa fedha kutoka serikali kuu kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 584.2.

Sauti ya afisa mtendaji

Ameongeza kwa kubainisha kuwa ujenzi wa shule hiyo ya sekondari utasaidia sana kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kuhudhuria masomo katika shule jirani za sekondari ikiwemo shule ya sekondari Nyamigota.

Afisa mtendaji wa kata ya Nyamigota akizungumzia ujenzi wa shule. Picha na Evance Mlyakado

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wametumia nafasi hiyo kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii huku wakisisitiza kuwa ujenzi wa shule hiyo katika kijiji chao ni majibu ya serikali kutokana na kilio chao cha muda mrefu cha kuomba shule ya sekondari katika eneo lao.

Sauti ya wananchi
Muonekano wa eneo la ujenzi wa shule baada ya kufanyiwa usafi wa wananchi. Picha na Evance Mlyakado