Ubovu wa barabara wakwamisha huduma za kijamii Songambele
8 April 2024, 9:59 pm
14 Kambarage ni miongoni mwa maeneo ambayo yanaendelea kushuhudia athari za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofautitofauti ya mkoa wa Geita na nchi nzima kwa ujumla.
Na kale Chongela
Wakazi wa Songambele mtaa wa 14 Kambarage kata ya Buhalahala mjini Geita wamedai kukabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara hali ambayo inakwamisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi.
Baadhi ya wakazi wa Songambele wamesema ubovu huo wa barabara unapelekea baadhi ya maji kuingia kwenye nyumba za watu kutokana na barabara hizo kukosa mitaro ya kusafirisha maji.
Aidha wananchi hao wameongeza kuwa kutokana na adha hiyo wanalazimika kuvua viatu hasa wakati wa mvua inaponyesha kwani inakuwa vigumu kutembea eneo hilo kutokana na maji kuingia kwenye makazi yao.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA wilaya ya Geita Mhandisi Bahati Subeya amekiri kuwepo kwa baadhi ya barabara kuharibiwa na mvua na kwamba ili kutatua changamoto hiyo tayari wameshaanza kupokea fedha za dharura ili kuboresha maeneo yaliyoharibiwa na mvua.