Taasisi ya mtetezi wa mama yawataka wajawazito kuacha kukimbilia kwa waganga wa kienyeji
29 October 2023, 2:03 pm
Imani potofu kwa wanawake wajawazito katika maeneo mengi ya vijijini wilayani Geita imetajwa kuwa sababu ya vifo vya mama na mtoto.
Na Mrisho Sadick:
Baadhi ya wanawake wajawazito katika Kata ya Nzera wilayani Geita wametakiwa kuachana na Imani potofu za kukimbilia kwa waganga wa kienyeji pindi wanapotaka kujifungua hali ambayo imekuwa ikisababisha vifo vya mama na mtoto kwa kiasi kikubwa.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mtetezi wa mama wilaya ya Geita katika Hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo Kata ya Nzera kufuatia kuwepo kwa namba kubwa ya wanawake hususani vijijini kuendelea kukumbatia mila potofu ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa ustawi wa Jamii.
Katibu msaidizi Midian Mussa na afisa habari Benson Alex wa taasisi hiyo wamesema taasisi hiyo imetembelea katika Hospitali hiyo kwa lengo la kufanya usafi, kuzungumza na wagonjwa pamoja na kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji.
Afisa mteknolojia wa maabara katika Hospitali hiyo Petty Mzumbwe amesema upungufu wa damu ni asilimia 95 huku Mganga Mfawidhi Shdrack Omega akiipongeza Taasisi hiyo kwa hatua hiyo nakuyaomba makundi mengine katika Jamii kuiga Mfano huo.