Storm FM
Storm FM
5 April 2026, 20:03

“Hii barabara imekuwa ikitupa usumbufu mkubwa sana kwahiyo imetulazimu kuweka mawe ili kuondoa usumbufu wakati wa kutumia” – Mwananchi
Na: Kale Chongela
Wananchi wa mtaa wa Nyantorotoro B, kata ya Nyankumbu, halmashauri ya Manispaa ya Geita, wameonesha mshikamano kwa kujitolea kushiriki katika uboreshaji wa sehemu korofi za barabara inayounganisha mtaa wa Nyantorotoro ubaoni hadi mtaa wa Mbabani.
Baadhi ya wananchi wakizungumza na Storm FM wamesema hatua hiyo imekuja kufuatia changamoto ya muda mrefu ya miundombinu mibovu, hasa kwa baadhi ya maeneo yalikuwa yakipitisha maji na kusababisha uharibifu wa barabara kwa watumiaji wa vyombo vya moto.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bw. Juma Ally amepongeza juhudi hizo za wananchi huku akibainisha kuwa ushirikiano huo ni mfano mzuri wa uzalendo na kujitolea katika kuleta maendeleo ya jamii.

Kaimu meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA Wilaya ya Geita Mhandisi Gadi Loi akizungumza kwa njia ya simu amekiri kuwepo wa changamoto hiyo na kueleza kuwa eneo hilo tayari wameliombea fedha kiasi cha shilingi milioni 170 kwaajili ya kuweka molamu.