Storm FM
Storm FM
28/03/2026, 12:49

Wakazi wa Kitongoji cha Elimu, Kijiji cha Kaboha wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wameipongeza serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa nishati ya umeme katika eneo hilo, hatua iliyosaidia kuondoa changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwenda vijiji jirani kufuata huduma za kukoboa mpunga na kusaga nafaka.
Mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambapo serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 17.77 kwa ajili ya kufikisha umeme katika vitongoji 15 kwa kila jimbo mkoani Geita
Na Mrisho Sadick – Geita
Kaimu meneja wa TANESCO Wilaya ya Nyang’hwale Richard Maduhu akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo iliyofika katika kitongoji cha elimu kukagua maendeleo yake amesema mpaka sasa vitongoji 8 kati ya 15 vimeshafikishiwa huduma hiyo na mradi huo umefikia asilimia 71.
Wakazi wa Kitongoji cha elimu wametoa pongezi hizo kwa kusema kuwa kabla ya mradi huo kufika katika kijiji hicho walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda vijiji jirani kutafuta huduma za kukoboa mpunga na kusaga nafasa lakini kwasasa huduma hizo zinapatikana kijijini humo.

Akiwa kwenye ziara hiyo mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame ameihakikishia CCM kuwa serikali itaendelea kuhakikisha kaya zote zinafikiwa na huduma ya umeme ili kuboresha maisha ya wananchi nakwamba kasi ya usambazaji inayoendelea kwenye vitongoji inakwenda sambamba na usambazaji wa huduma hiyo kwenye taasisi za umma , binafsi kaya, sehemu za uzalishaji na kaya.

Wakati huohuo, Kamati hiyo ya Siasa pia imetembelea mradi wa maji katika kijiji cha Lubando Kata ya Shabaka unaohusisha uchimbaji wa visima vitano katika vijiji vitano vya jimbo hilo, Meneja wa RUWASA wilaya hiyo Suzana Mabula amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni milioni 300.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nyang’hwale Alhaji Adam Mtore ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopitiwa na kamati ya siasa huku akiwataka wananchi kuendelea kuilinda na kuitunza miradi hiyo kwa manufaa yao kwakuwa serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza kwenye miradi hiyo.