Storm FM

Diwani wa kata ya Ichwankima ashukuru wajumbe ahimiza umoja

15 February 2026, 12:44 am

Diwani wa kata ya Ichwankima, Kulwa Elias Ludohe akizungumza katika mkutano maalumu alioandaa. Picha na Ester Mabula

“Maendeleo ya kata yetu yanahitaji umoja na ushirikiano na tuweke makundi pembeni, na mimi nawahakikishia nitakuwa kiongozi wa wote bila kumbagua mtu” – Diwani Kulwa Ludaho

Na: Ester Mabula

Diwani wa Kata ya Ichwankima Kulwa Elias Ludaho iliyopo wilaya ya Chato katika jimbo la Chato kaskazini mkoani Geita, amefanya mkutano mkuu wa chama wa kata na wanachama wa CCM kwa lengo la kuwashukuru kwa kumchagua kutumikia kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Februari 14, diwani huyo amewashukuru wanachama na wananchi kwa imani kubwa waliyoionesha kwake akieleza atawatumikia wote bila kuwa na ubaguzi.

Sauti ya diwani, Kulwa Elias Ludohe

Mgeni rasmi katika mkutano huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Chato Dotto Mazuri, aliwahimiza wanachama kuendelea kudumisha umoja na mshikamano huku akiwahimiza wananchi kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita ili kujikinga na gharama kubwa za matibabu  pindi wapatapo maradhi.

Sauti ya mgeni rasmi, Dotto Mazuri
Mgeni rasmi, Katibu wa CCM wilaya ya Chato Dotto Mazuri akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano (hawapo pichani). Picha na Ester Mabula

Katika hatua nyingine, mgeni maalumu ambaye ni mbaraza na diwani wa kata ya Kalangalala, Reuben Sagayika amechangia kiasi cha shilingi laki tatu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama katika kata hiyo huku wajumbe waliohudhuria mkutano huo wakiahidi ushirikiano kwa diwani wa kata hiyo ili kuchochea maenedeleo.

Sauti ya Mbaraza, Reuben Sagayika

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa chama ngazi ya matawi, kijiji, kata na wilaya  ambapo ulihitimishwa kwa viongozi waliofanya vizuri katika uchaguzi mkuu kwenye kata hiyo kupewa vyeti vya pongezi ambapo baadhi ya wajumbe wamempongeza diwani na kueleza wana matarajio makubwa ndani ya miaka mitano.

Sauti ya wajumbe na viongozi wa CCM
Baadhi ya wajumbe na viongozi wa CCM ngazi ya matawi, vijiji na kata waliohudhuria mkutano huo. Picha na Ester Mabula