Storm FM
Storm FM
14 February 2026, 1:16 am

Ziara hiyo imekagua miradi ya BOOST iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa. BOOST ni sehemu ya mpango wa lipa kulingana na matokeo katika elimu awamu ya pili (EPforR II) na inachangia utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa sekta ya elimu wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/26.
Na: Ester Mabula
Diwani wa Kata ya Kalangalala Mhe. Reuben Sagayika, Februari 13, 2026, akiwa na kamati ya maendeleo ya kata pamoja na viongozi wa serikali ya mtaa wa Mbugani amefanya ziara ya kutembelea shule tatu za msingi zilizopo katika mtaa huo ambazo ni Mbugani, Umoja na Kivukoni kwa lengo la kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia mpango wa BOOST.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani Sagayika amesema lengo la ziara hiyo ni kufatilia maendeleo ya miradi sambamba na kukagua eneo jipya litakalotumika kujenga sekondari katika mtaa wa Mbugani

Kwa upande wake, kaimu Afisa elimu kata ya Kalangalala Mwl. Regina Ketau amepongeza uwepo wa ziara hiyo akieleza itaongeza chachu ya uwajibikaji huku walimu wakuu wa shule zilizotembelewa wakibainisha manufaa ya miradi hiyo katika shule zao.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mbugani ambapo zinapatikana shule hizo Bw. Jumanne Bayasabe amesema katika kuboresha hali ya ufaulu ataendelea kuhimiza wazazi kushiriki kwenye suala la upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi pindi wawapo shuleni.

Ziara hiyo imehitimishwa kwa Diwani Sagayika kusisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu hadi miradi yote itakapokamilika, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na watendaji katika kuchagiza maendeleo ya kata hiyo.
