Storm FM
Storm FM
26 January 2026, 5:42 pm

Kutokana na mvua za El nino zilizonyesha siku za nyuma serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kukabiliana na athari za uharibifu huo katika maeneo mbalimbali nchini.
Na Mrisho Sadick:
Wakazi wa Kata ya Iponya wilayani Mbogwe mkoani Geita wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha ujenzi wa daraja kubwa katika Mto Buluhe, eneo ambalo hapo awali walilazimika kutumia mitumbwi kuvuka. Hali hiyo ilisababisha vifo vya wananchi pamoja na upotevu wa mazao baada ya kusombwa na maji wakati wa mvua kubwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya dharura ya ujenzi wa madaraja na barabara zinazojengwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12, miradi hiyo inahusisha barabara ya Wendele–Mlele katika maeneo ya Kanegere na Lubeho pamoja na barabara ya mkoa ya Kashelo–Masumbwe na Mwabomba.

Akiwa katika Kata ya Iponya kwenye ujenzi wa daraja linalounganisha mikoa ya Geita na Shinyanga, wakazi wa eneo hilo wamesimulia madhila waliyokuwa wakikumbananayo kabla ya uwepo wa daraja hilo, ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita Mhandisi Vedastus Maribe amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 90, likijengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.9, lina midomo 15 na lina upana wa mita nne kwa mita tatu, huku likitarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa usafiri na usalama wa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Godfrey Kasekenya, amesema kazi iliyofanyika wilayani Mbogwe ni sehemu ya juhudi za serikali zilizotekelezwa nchi nzima kufuatia mvua kubwa za El Niño zilizosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja nakwamba serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kukabiliana na athari za uharibifu huo katika maeneo mbalimbali nchini.