Storm FM

Wanafunzi 261 hawajaripoti shule Katoro

25 January 2026, 2:51 pm

Wanafunzi wa shule ya sekondari Sabila walipotembelewa na Jumuiya ya wazazi Kata ya Katoro. Picha na Mrisho Sadick

Hadi sasa wanafunzi 480 pekee ndio walioripoti katika shule hizo tatu, huku idadi kubwa ya wanafunzi waliopangiwa kujiunga bado hawajafika.

Na Mrisho Sadick:

Jumla ya wanafunzi 261 kati ya 741 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule tatu za Sekondari za Kata ya Katoro wilayani Geita bado hawajaripoti shuleni, hali iliyozua wasiwasi miongoni mwa wadau wa elimu huku jitihada za kuwatafuta wanafunzi hao na kubaini walipo zikiendelea.

Kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Katoro imefanya ziara maalum katika shule za Sekondari Kaduda, Shigongo na Sabila kwa lengo la kukagua mwitikio wa wanafunzi walioripoti, changamoto zilizopo pamoja na kutoa hamasa kwa wazazi na wanafunzi kuhakikisha wanazingatia umuhimu wa elimu.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Kaduda walipotembelewa na Jumuiya ya wazazi ya CCM. Picha na Mrisho Sadick

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Katoro, amesema hadi sasa wanafunzi 480 pekee ndio walioripoti katika shule hizo tatu, huku idadi kubwa ya wanafunzi waliopangiwa kujiunga bado hawajafika shuleni, jambo linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, viongozi wa kata na jamii kwa ujumla.

Sauti ya Mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi Katoro

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Katoro, Zubeda Hamis Mussa, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kuwa changamoto za kiuchumi haziwi kikwazo kwa watoto wao kupata elimu, akisisitiza kuwa elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtoto na jamii kwa ujumla. Ameeleza kuwa ofisi yake ipo tayari kushirikiana na wazazi katika kuwasaidia wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto ikiwemo kukosa sare za shule na vifaa muhimu vya masomo.

Sauti ya Diwani wa Katoro
Wanafunzi wa shule ya sekondari Shigongo walipotembelewa na Jumuiya ya wazazi ya CCM Kata ya Katoro. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wao, wakuu wa shule hizo tatu wamesema bado wanaendelea na jitihada za kufuatilia wanafunzi ambao hawajaripoti kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji, watendaji wa kata pamoja na wazazi, ili kuhakikisha kila mwanafunzi aliyepangiwa anaanza masomo kwa wakati.

Sauti ya wakuu wa shule

Wakati huo huo, wanafunzi wa shule ya Sekondari Kaduda ambao walifanya vizuri katika matokeo ya kidato cha pili na kuiwezesha shule hiyo kushika nafasi ya pili wilayani Geita, wamesema kuwa motisha kutoka kwa viongozi, walimu na wazazi imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza bidii katika masomo, hali ambayo wanaiomba iendelee ili kuimarisha zaidi ufaulu na nidhamu shuleni.