Storm FM
Storm FM
23 January 2026, 7:34 pm

“Ziara hii imekuwa ni bora sana kwetu na yenye tija kwani itatuwezesha kuelewa kwa upana shughuli zinazofanyika ndani ya mgodi” – Diwani Sagayika
Na: Ester Mabula
Kamati ya maendeleo ya kata ya Kalangalala, halmashauri ya manispaa ya Geita ikiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Reuben Emmanuel Sagayika, leo Januari 23, 2026, imefanya ziara maalumu ya kutembelea mgodi wa Geita Gold Mine (GGML) uliopo halmashauri ya manispaa ya Geita mkoani Geita.
Ziara hiyo imelenga kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali za uchimbaji madini pamoja na mchango wa mgodi huo katika maendeleo ya jamii zinazouzunguka.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani Sagayika amesema lengo kuu la kamati ni kupata uelewa wa kina kuhusu uendeshaji wa mgodi, fursa za ajira kwa wananchi wa eneo hilo, pamoja na miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) inayotekelezwa na GGML.

Kwa upande wao, viongozi na wataalamu kutoka GGML waliipokea kamati hiyo na kutoa maelezo kuhusu historia ya mgodi, teknolojia zinazotumika katika uchimbaji wa madini, hatua za usalama kazini, pamoja na jitihada zinazochukuliwa kulinda mazingira.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Kalangalala, kwani itasaidia kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu shughuli za mgodi huo na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali ya kata na mgodi wa GGML kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii.
