Storm FM
Storm FM
21 January 2026, 4:11 pm

Siku ya kwanza ya uzinduzi wa zoezi hili imepandwa miti zaidi ya 10,000 katika taasisi za umma na binafsi pamoja na majumbani.
Na Mrisho Sadick:
Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita mkoani Geita, imezindua kampeni maalum ya upandaji wa miti zaidi ya laki tano (500,000) katika taasisi mbalimbali pamoja na makazi ya wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Januari 21,2026 katika Shule ya Sekondari Mkolani, ukiongozwa na Diwani wa Kata ya Nyankumbu Paschal Kimisha Sukambi ambaye amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kulinda mazingira na kuhakikisha ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Nyankumbu Alfred Lameck amesema licha ya miti hiyo kupandwa katika taasisi za umma kama shule na ofisi za serikali kila kaya imetakiwa kupanda angalau miti mitatu na kuitunza ili kuhakikisha inaleta tija iliyokusudiwa.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo Esther Selemani amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii nzima katika uhifadhi wa mazingira, akieleza kuwa kampeni hiyo itaongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkolani Daniel Mwita amesema shule hiyo imepokea miche zaidi ya 2,000 kwa ajili ya zoezi la upandaji, na kuahidi kuitunza ili kufanikisha malengo ya kampeni hiyo huku wanafunzi wa shule hiyo wameeleza kufurahishwa na zoezi hilo wakisema litawajengea utamaduni wa kutunza mazingira tangu wakiwa shuleni.
Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa walioshiriki katika zoezi hilo Henry Tito wa mtaa wa Nyamakale na Hassan Ally mwenyekiti wa mtaa wa Buchundwankende wamesema kampeni hiyo itasaidia kurejesha uoto wa asili na kupunguza athari za ukame katika maeneo yao.

Kampeni hiyo ya upandaji miti inatarajiwa kuendelea katika kata nzima ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Manispaa ya Geita wa kulinda mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi huku ikiongozwa na kaulimbiu isemayo Nyankumbu ya kijani inaanza na mimi.