Storm FM

Vijana zaidi ya 400 wakutana kujadili fursa na mkuu wa wilaya Nyang’hwale

17 January 2026, 5:08 pm

Baadhi ya vijana wakiwa katika kongamano la vijana wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Wilaya ya Nyang’hwale yenye wakazi 225,803 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ina makadirio ya vijana zaidi ya 90,000.

Na Mrisho Sadick

Zaidi ya vijana 400 kutoka Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita wamekutana katika kongamano maalum lililoandaliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Grace Kingalame, kwa lengo la kusikiliza na kujadili fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo wilayani humo pamoja na changamoto zinazowakabili vijana.

Wilaya hiyo imebainika kuwa na fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, uchimbaji wa madini ya dhahabu pamoja na shughuli za ujasiriamali. Kongamano hilo ni miongoni mwa makongamano matano yaliyoandaliwa wilayani humo kwa lengo la kuwawezesha na kuwaunganisha vijana na fursa za maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame akizungumzia madhumuni ya kongamano hilo. Picha na Mrisho Sadick

Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Msalala Januari 16,2026 Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kwa bidii na ubunifu, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ujasiriamali huku akiahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kutatua changamoto zinazowakabili vijana, hususan katika maeneo ya mitaji, elimu ya ujasiriamali na ajira.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye kongamano la vijana wilayani Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Afisa Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Nyang’hwale Ushuda Kibona amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu kwa vijana kujifunza, kubadilishana uzoefu na kupata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo, hususan katika kilimo cha kisasa, ufugaji na mikopo ya vikundi vya vijana.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Nyang’hwale Estelina Thobias amebainisha kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na makundi ya vijana katika kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kuendeleza miradi ya kiuchumi yenye tija.

Sauti ya Ripoti ya Stori na Mrisho Sadick