Storm FM
Storm FM
15 January 2026, 4:39 pm

Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni tukio hilo la kushangaza limewaacha wakazi wa mtaa huo katika hali ya taharuki.
Na Mrisho Sadick:
Moto wa ajabu umezikumba familia mbili katika mtaa wa Nyantorotoro Kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita Mkoani Geita huku wakazi wa eneo hilo wakiiomba serikali kuingilia kati kwani matukio hayo yamezua taharuki.
Wahanga wa tukio hilo wamelazimika kuzikimbia nyumba zao na kuanza kulala nje au kwa majirani kwa kuhofia usalama wa maisha yao, wakieleza kuwa moto huo umekuwa ukiwaka ghafla bila chanzo cha kawaida kinachofahamika.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuingilia kati sakata hilo, huku baadhi ya wakazi wakidai kuwa huenda chanzo cha matukio hayo kinahusishwa na imani za kishirikina, madai yaliyozidi kuongeza hofu na sintofahamu katika jamii.

Viongozi na wakazi wa mtaa wa Nyantorotoro wamesema matukio hayo yamewavuruga kisaikolojia na kuathiri maisha yao ya kila siku, wakisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuwahakikishia usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumza kuhusu tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita Shabani Hamis Dawa amesema jeshi hilo limefika eneo la tukio na kuanza uchunguzi wa kina, akibainisha kuwa moto huo unaonekana kuwa wa ajabu na haujafanana na matukio ya kawaida ya moto nakwamba uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu, kutoa ushirikiano na kuepuka kueneza uvumi unaoweza kuongeza taharuki wakati serikali ikiendelea kufuatilia kwa karibu sakata hilo.