Storm FM
Storm FM
15 January 2026, 4:19 pm

Leo ni siku ya pili tangu kuanza kwa muhula mpya wa masomo ambapo shule zimefunguliwa Januari 13, 2026 kote nchini.
Na: Ester Mabula
Diwani wa Kata ya Nyanguku ambaye pia ni Naibu Meya wa halmashauri ya manispaa ya Geita amewaasa wazazi na walezi kujiepusha na vitendo vya kuwakatisha masomo watoto wao na badala yake wawapeleke shule ili wapate elimu.
Mhe. Ngole ametoa kauli hiyo leo Januari 15, 2026 akiwa katika shule ya sekondari Nyanguku iliyopo halmashauri ya manispaa ya Geita, ambapo amekuwa na utaratibu wa kukabidhi madaftari kwa wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza wanaojiunga katika shule hiyo.

Amewasisitiza wazazi kuacha tabia ya kuwaozesha mabinti sambamba na kuhusisha watoto na shughuli za kilimo, akisema mustakabali wa maendeleo duniani kote unategemea elimu.
Baadhi ya wazazi waliopeleka watoto wao katika shule hiyo Onesmo Mashishanga na Getruda Stephano wamemshukuru Diwani huyo kwa kuendelea kuwasadia wazazi kununua madaftari wakisema hatua hiyo inaleta motisha zaidi.

Afisa elimu kata ya Nyanguku Innocent Yasese amesema Jumla ya wanafunzi 90 wa kidato cha kwanza wameripoti shuleni hapo kuanza kidato cha kwanza ambapo amesema hatua hiyo ya kutoa madaftari inayofanywa na diwani inaongeza motisha ya wanafunzi kusoma.
