Storm FM
Storm FM
9 January 2026, 4:37 pm

Zaidi ya wanafunzi 5,700 kutoka shule saba za msingi na shule moja ya sekondari ndio wanufaika wa moja kwa moja wa mpango huo.
Na Mrisho Sadick:
Kata ya Shabaka wilayani Nyang’hwale mkoani Geita imelima jumla ya ekari 41 za mahindi na viazi lishe ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale wa kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa chakula mashuleni kwa mwaka mzima.
Akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mpango huo katika Kata zote Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame akiwa katika Kata ya Shabaka amesema zoezi hilo linafanyika katika shule zote 74 za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Kata ya Shabaka amesema zaidi ya wanafunzi 5,700 kutoka shule saba za msingi na shule moja ya sekondari ndio wanufaika wa moja kwa moja wa mpango huo huku Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo amesema mpango huo umeanza kuonesha matokeo chanya tangu ulipoanza kutekelezwa.

Mkuu wa wilaya kwa kushirikiana na mkurugenzi wa halmashauri wamenunua mbegu kilo zaidi ya1,400 kupitia mapato ya ndani nakuzigawa kwenye shule zote kwa wastani wa kilo 16 kila shule kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ambao umefanikiwa kwa asilimia kubwa.