Storm FM
Storm FM
9 January 2026, 4:09 pm

Mtaa wa Ilungwe unakadiriwa kuwa na idadi ya wakazi zaidi ya 1,500 wanaotegemea huduma za elimu katika mtaa wa Nyamakale ambao upo zaidi ya kilometa tatu.
Na Mrisho Sadick:
Wakazi wa Mtaa wa Ilungwe Kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita wamehamasika kuanzisha ujenzi wa shule ya msingi katika eneo hilo ili kuwanusuru watoto wao na ajali kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata elimu mitaa jirani.
Wakizungumza kwa hamasa kubwa leo Januari 09,2026 baadhi ya wakazi wa mtaa huo waliojitokeza kwa wingi kusafisha eneo ambapo shule hiyo itajengwa wamesema hatua hiyo itakwenda kuondoa Safari isiyo na uhakika wa usalama, iliyojaa hatari za ajali na uchovu kwa watoto.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo Daud Mwanzalima na Afisa mtendaji wa Kata ya Nyankumbu Alfred Lameck wamesema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kutatoa fursa kwa watoto wengi kupata elimu bora karibu na makazi yao.

Diwani wa Kata ya Nyankumbu ambae ameongoza zoezi hilo amesema atahakikisha anasukuma ajenda hiyo ya ujenzi wa shule ili ikamilike haraka ili kuwanusuru watoto ambao wanatembea umbali wa zaidi ya kilometa tatu kwenda katika shule za jirani hali ambayo ni hatari kwa usalama wao wawapo barabarani.