Storm FM

Nyang’hwale yasisitiza matumizi ya teknolojia kukuza biashara

8 January 2026, 11:36 am

Viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na wanufaika wa mikopo. Picha na Mrisho Sadick

Ucheleweshaji wa marejesho una punguza juhudi za serikali kuendelea kutoa fedha za mikopo kwa vikundi vingine.

Na Mrisho Sadick:

Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kutumia teknolojia ya mawasiliano ikiwemo mitandao ya kijamii kama nyenzo muhimu ya kutangaza, kukuza na kuongeza tija ya biashara zao.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bi Husna Toni Januari 07,2025 katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi 34 vya Wanawake , Vijana na watu wenye ulemavu yenye jumla ya shilingi milioni 300, ikiwa ni awamu ya pili ya utoaji wa mikopo hiyo, zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Bi Grace Kingalame katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari msalala wilayani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bi Husna Toni akizungumza kwenye hafla ya utoaji mikopo. Picha na Mrisho Sadick
Sauti ya Mkurugenzi Nyang’hwale

Mratibu wa mikopo wilaya ya Nyang’hwale Yahaya Selemani akitoa taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo amesema vikundi vya wanawake 13 vimepatiwa milioni 72, vikundi 15 vya vijana vimepatiwa milioni 207 na vikundi vya watu wenye ulemavu 6 vimenufaika na shilingi milioni 20 huku akielezea ucheleweshaji wa marejesho una punguza juhudi za serikali kuendelea kutoa fedha za mikopo kwa vikundi vingine nakwamba wanaendelea kushirikiana na kamati za mikopo ngazi ya Kata na vijiji kuhakikisha fedha zote zilizokopwa zinarejeshwa.

Sauti ya mratibu wa mikopo Nyang’hwale
Miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 wilaya ya Nyang’hwale . Picha na Mrisho Sadick

Naye afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Nyang’hwale Estelina Thobias amesema kuwa hali ya marejesho ya mikopo inaendelea kuimarika baada ya kuundwa kwa timu maalumu ya ufuatiliaji na utoaji wa elimu kwa vikundi, ameeleza kuwa deni la mikopo ya zamani lililokuwa shilingi milioni 150 sasa limepungua hadi kufikia shilingi milioni 132, hatua inayoashiria mwamko mzuri kwa wanufaika.

Sauti ya afisa maendeleo ya Nyang’hwale

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyang’hwale Ali Haji Adam Mtore amewakumbusha wanufaika wa mikopo hiyo kuzingatia matumizi sahihi ya fedha kwa kuendana na kipato chao halisi ili kuepuka changamoto ya kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo John Isack amesema wataendelea kuongeza nguvu ya makusanyo ya mapato ya ndani ili kuhakikisha kila robo ya mwaka wanatoa mikopo.

Sauti ya mwenyekiti wa CCM na Halmashauri ya Nyang’hwale
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame akizungumza kwenye hafla ya utoaji wa mikopo. Picha na Mrisho Sadick

Akihitimisha hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame, amewahimiza wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua kiuchumi, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni njia mojawapo ya kumpa imani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale