Storm FM
Storm FM
5 December 2025, 2:25 pm

Changamoto zilizokuwa kikwazo mwaka Jana ikiwemo wazazi kuwalazimisha watoto kufeli, ukosefu wa chakula shuleni pamoja na baadhi ya wadau kutowajibika ipasavyo.
Na Mrisho Sadick:
Ufaulu wa mtihani wa darasa la saba katika Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita umeongezeka kutoka asilimia 53.7 mwaka jana hadi asilimia 69.9 mwaka huu ikiwa ni matokeo ya mikakati madhubuti iliyowekwa kukabiliana na hali ya ufaulu duni iliyojitokeza mwaka uliopita.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale Husna Toni akiwa kwenye hafla ya utoaji wa zawadi kwa walimu, wanafunzi na viongozi waliofanikisha mafanikio hayo Disemba 04,2025 wilayani humo amesema hatua hiyo imechangiwa na usimamizi thabiti wa changamoto zilizokuwa kikwazo mwaka Jana ikiwemo wazazi kuwalazimisha watoto kufeli, ukosefu wa chakula shuleni pamoja na baadhi ya wadau kutowajibika ipasavyo huku katibu tawala wilayani humo akiwaomba madiwani kuweka mikakati ya kuondoa utoro shuleni.

Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo amesema Halmashauri ilitenga zaidi ya milioni 20 kama motisha kwa walimu, wanafunzi na viongozi waliofanikisha ufaulu huo huku akisisitiza kuwa ahadi hiyo imetekelezwa kikamilifu ili kuendeleza ari ya kufanya vizuri zaidi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Mohammed Gombati ameridhia kuanzishwa kwa mfuko maalumu utakaosaidia wanafunzi wanaokumbana na changamoto wanapohitaji kusafiri nje ya mkoa kwa masuala ya kielimu ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekwamishwa na mazingira magumu.

Wanafunzi na wazazi wilayani Nyang’hwale wamepongeza mikakati iliyowekwa nakufanikisha ufaulu huo huku wakiiomba serikali kuendelea kuwachukulia hatua kali baadhi ya watu ambao wanaleta mchezo kwenye suala la elimu.