Storm FM
Storm FM
1 December 2025, 2:14 pm

Changamoto mbalimbali zinazokabili chuo hicho ikiwemo ukosefu wa uzio unaohatarisha mali za chuo, upungufu wa zana za kisasa za mafunzo.
Na Mrisho Sadick:
Taasisi za serikali na zile za binafsi wilayani Geita zimetakiwa kuwapa kipaumbele vijana waliohitimu mafunzo ya Ufundi Stadi kupitia VETA Mkoa wa Geita kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kupunguza wimbi la changamoto ya ajira linalowakabili vijana nchini.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba wakati wa mahafali ya kwanza ya Chuo cha ufundi stadi VETA Manispaa ya Geita amesema kuwa miradi mingi inayotekelezwa katika Halmashauri na taasisi nyingine imekuwa ikihitaji mafundi wenye ujuzi wa kati hivyo kuwajumuisha wahitimu wa VETA katika miradi hiyo kutasaidia si tu kupunguza ukosefu wa ajira, bali pia kuboresha ubora wa kazi zinazotekelezwa katika jamii.

Mkuu wa chuo hicho Tadeus Panga amesema kuwa kwa sasa chuo kinatoa kozi tano na kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 900 kwa kozi fupi na 520 kwa kozi ndefu, fani zinazotolewa kwa sasa ni Ufundi Bomba, Umeme wa Majumbani, Uhazili na Kompyuta, Upishi, na Umeme wa Magari

Panga ameeleza changamoto mbalimbali zinazokabili chuo hicho ikiwemo ukosefu wa uzio unaohatarisha mali za chuo, upungufu wa vifaa vya kisasa vya mafunzo , ukosefu wa magari kwa ajili ya mafunzo huku akiiomba serikali na wadau wa elimu mkoani Geita kuona namna ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuongeza ufanisi katika kujifunza.
Vijana waliohitimu mafunzo hayo wameahidi kutumia ujuzi walioupata kujiajiri, na kuanzisha miradi midogo ya biashara, hatua ambayo si tu itawasaidia kiuchumi, bali pia itachangia maendeleo ya jamii na kuongeza wigo wa ajira kwa wengine.
