Storm FM
Storm FM
1 December 2025, 1:40 pm

Mtandao huo umefanikisha ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari Kasamwa ikiwemo chumba maalumu kwa ajili ya wasichana watakapokuwa wakati wa hedhi.
Na Mrisho Sadick:
Mtandao wa marafiki wa elimu Kanda ya Ziwa umetoa msaada wa chakula kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Neema House , Meza na Viti kwa ajili ya shule ya msingi Nyantindili iliyopo Kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa viti na Meza kwa ajili ya walimu.
Mtandao huo umetoa vifaa hivyo baada ya kumaliza mkutano wake mkuu wa mwaka ulioketi mkoani Geita, akizungumza mara baada ya kupokea viti hivyo Mwalimu mkuu wa shule hiyo amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto kwa walimu.
Mwenyekiti wa marafiki wa elimu kanda ya ziwa Chrisant Nyakita amesema katika msaada huo wametoa meza mbili na viti sita pamoja na vyakula nakwamba wataendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu.

Nae mkurugenzi wa marafiki wa elimu Mkoa wa Geita Ayubu Bwanamad amesema mtandao huo umefanikisha ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari Kasamwa ikiwemo chumba maalumu kwa ajili ya wasichana watakapokuwa wakati wa hedhi pamoja na ujenzi wa vyoo shule ya msingi Mwatulole Manispaa ya Geita.

Afisa elimu mkoa wa Geita Antony Mtweve akizungumza kwaniaba ya katibu tawala mkoa wa Geita ameupongeza mtandao huo wa marafiki wa elimu kwa kuendelea kusaidia kutatua changamoto huku akiahidi serikali kuendelea kuwaunga mkono.