Storm FM

Jumla ya wanafunzi 607 wafadhiliwa shule za WAJA

30 November 2025, 5:33 am

Mkuu wa mkoa wa Geita mhe. Reuben Martine Shigela akiwa katika sherehe ya mahafali ya shule za WAJA. Picha na Ester Mabula

“Hata mimi nilikuwa kama nyie miaka 31 iliyopita, ni muhimu kuwa na nidhamu na kuishi katika ndoto zenu huku mkiwaheshimu watu wote kwenye Jamii” – RC Shigela

Na: Ester Mabula

Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Reuben Shigela amewataka wahitimu wa kidato cha nne katika shule za WAJA (Wasichana na Wavulana) kuzingatia mafunzo ya kielimu waliyopata kwa miaka minne sambamba na kuishi katika ndoto zao pindi wanaporejea majumbani kwa wazazi wao.

RC Shigela ametoa rai hiyo Novemba 29, 2025 katika sherehe ya mahafali iliyofanyika katika shule ya wasichana ya Waja iliyopo manispaa ya Geita na kusisitiza kuwa hata yeye aliishi katika maono aliyoamini huku akiwa na juhudi na nidhamu.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe Martine Shigela
Mkurugenzi mkuu wa shule za WAJA ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Mhandisi Chacha Wambura. Picha na Ester Mabula

Mkurugenzi mkuu wa shule hizo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Mhandisi Chacha Mwita Wambura amewashukuru wazazi kwa kuziamini shule za Waja huku akiwasihi wahitimu kuzingatia maadili waliyofundishwa shuleni sambamba na kuwa na nidhamu kwa watu wote kwenye jamii.

Sauti ya Mkurugenzi mkuu wa shule za WAJA, Mhandisi Chacha Wambura

Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, mkuu wa shule ya wasichana ya Waja ameeleza kuwa shule hizo zimeweza kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 607 tangu mwaka 2014 huku akieleza kuwa uwepo wa miundombinu bora na rafiki inawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo jambo ambalo linachochea zaidi ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Sauti ya Mkuu wa shule ya wasichana ya WAJA
Wahitimu wa shule ya wasichana ya WAJA wakiwa katika sherehe ya mahafali. Picha na Ester Mabula

Aidha baadhi ya walimu waliofanya vizuri kwa kuwa na ufaulu mzuri wa wanafunzi kwenye masomo yao wamepewa zawadi ya pikipiki ili kuongeza chachu ya ufundishaji sambamba na kuongeza hari ya ufaulu kwa wanafunzi.

Mwalimu wa somo la hisabati shule ya wavulana WAJA akikabidhiwa zawadi ya pikipiki kwa kupata ufaulu mzuri kwa mwaka 2024. Picha na Ester Mabula