Storm FM

Magonjwa yasiyoambukiza bado kitendawili Geita

26 November 2025, 6:08 pm

Zoezi la upimaji magonjwa yasioambukizi likiendelea katika mji mdogo wa Katoro. Picha na Mrisho Sadick

Tafiti zinaonesha kuwa Kwenye watu 100 watu 9 hadi 10 wanaugonjwa wa kisukari nchini huku jamii ikisisitizwa kuendelea kupima afya zao mara kwa mara.

Na Mrisho Sadick:

Zaidi ya watu 500 kutoka maeneo mbalimbali ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita Mkoani Geita wamejitokeza kupima magonjwa yasiyoambukiza huku idadi kubwa wakibainika kuwa na shinikizo la Juu la damu pamoja na kisukari.

Zoezi hilo limeendeshwa na Chama Cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa siku mbili katika viwanja vya mnada wa zamani Katoro huku mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Mkoa wa Geita Groly Temba amesema takwimu za mwaka Jana katika zoezi la aina hiyo shinikizo la juu  la damu liliongoza kwa asilimia 59 na kisukari asilimia 5.7 nakwamba mwaka huu kumekuwa na mafanikio makubwa.

Zoezi la upimaji magonjwa yasioambukizi likiendelea katika mji mdogo wa Katoro. Picha na Mrisho Sadick

Mratibu wa elimu ya afya kwa umma mkoa wa Geita Pascazia Madulu amesema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwemo ya kupuuza baadhi ya tamaduni kuwa magonjwa yasioambukiza yanatokana na kurogwa huku akiwasisitiza wananchi kuendelea kujitokeza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupima afya zao.

Mashombo Mkamba Kutoka makao Makuu ya Chama Cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania akizungumzia suala hilo. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Mashombo Mkamba Kutoka makao Makuu ya Chama Cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania amesema tafiti zinaonesha kuwa Kwenye watu 100 watu 9 hadi 10 wanaugonjwa wa kisukari huku watu asilimia 33% wanafariki kutokana na magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma hiyo wamekipongeza Chama Cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania kwa kuendelea kuwathamini kwakutoa huduma hiyo Bure huku wakiwataka Wananchi kuendelea kuchangamkia fursa hiyo pindi watakapofikiwa.

Sauti ya Ripoti hii na Mrisho Sadick