Storm FM
Storm FM
25 October 2025, 8:28 pm

Kupitia programu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale imefanikiwa kukopesha vikundi 114 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwa jumla ya shilingi milioni 674.5
Na Mrisho Sadick:
Watu wenye ulemavu wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wameendelea kunufaika na mpango wa mikopo ya asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha sera za uwezeshaji wananchi kiuchumi kwakuwa mikopo hiyo imekuwa mwanga wa matumaini kwao.
Wakizungumza katika hafla maalum ya utoaji wa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 206 kwa vikundi 31 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wanufaika hao wameeleza kuwa mikopo hiyo itawawezesha kupanua biashara zao za ufugaji wa kuku, uchomeleaji na kilimo cha kisasa huku wakiahidi kutumia fedha hizo kwa uaminifu na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili wengine nao wapate fursa ya kunufaika.

Afisa maendeleo wilayani humo Estelina Colman amesema vikundi vilivyopata mikopo vimepitiwa kwa makini na kuthibitishwa kuwa vimekidhi vigezo huku Katibu Tawala wa Wilaya Bi Kaunga Amani amesema serikali imeweka miongozo mipya yenye lengo la kuongeza uwajibikaji ikiwemo ukomo wa vikundi kukopa mwisho mara tatu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi Husna Tony amewahimiza wanufaika wa mikopo hiyo avikundi kujiunga na mfumo wa manunuzi wa serikali (NEST) ili kupata fursa zaidi za kufanya kazi na serikali huku Mkuu wa Wilaya ya Nyangh’wale Bi Grace Kingalame akitoa maagizo kwa maafisa maendeleo vijijini kuendelea kutoa elimu kwa wanavikundi wapya ili kuhakikisha wanafahamu taratibu na vigezo vya kupata mikopo hiyo.