Storm FM
Storm FM
18 October 2025, 9:12 pm

Hatua hiyo inalenga kurejesha mamlaka ya kiuchumi mikononi mwa wananchi na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wengi badala ya wachache.
Na Mrisho Sadick:
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ADA TADEA, Georges Busungu, amesema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha migodi mikubwa ya madini nchini inamilikiwa na kuendeshwa na Watanzania.
Busungu ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita mkoani Geita ambapo amesema hatua hiyo inalenga kurejesha mamlaka ya kiuchumi mikononi mwa wananchi na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wengi badala ya wachache. Amesema kuwa kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa watazamaji katika sekta ya madini, licha ya kuwa ndiyo wamiliki halali wa ardhi na rasilimali zilizomo.

Katika mkutano huo Katibu Mkuu wa ADA TADEA Salehe Msumali amesisitiza kuwa serikali ya chama hicho itasimamia kwa dhati maslahi ya wachimbaji wadogo na kuweka mazingira rafiki ya kisheria na kifedha ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini.

Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Simiyu Luhende Mipawa amewataka wananchi kuwa na imani na ADA TADEA akisema ni chama pekee kinachokuja na dira mpya ya kiuchumi inayolenga kujenga uchumi shirikishi unaowahusisha wananchi wote kuanzia ngazi ya chini.
Wananchi wa Geita waliohudhuria mkutano huo wameonesha kufurahishwa na sera hiyo, wakisema kuwa wanufaika wa kwanza watakuwa ni Watanzania wenyewe, hususan vijana wanaohangaika kutafuta ajira na wachimbaji wadogo wanaokumbwa na changamoto nyingi za mitaji na masoko.
Kwa mujibu wa sera hizo, serikali chini ya ADA TADEA itaunda mamlaka mahsusi ya kitaifa ya usimamizi wa madini yenye jukumu la kuhakikisha faida za sekta hiyo zinatiririka moja kwa moja kwa wananchi kupitia miradi ya kijamii kama elimu, afya, maji safi, na ujenzi wa miundombinu.