Storm FM

EAGT Nazareth Stamico kuanzisha miradi ya afya na elimu

16 October 2025, 8:48 am

Mwenyekiti wa kamati ya ununuzi wa kiwanja akikabidhi mkataba wa manunuzi kwa mchungaji wa EAGT Nazareth. Picha na Mrisho Sadick

Ujenzi wa hospitali hiyo ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma zinazotolewa na kanisa hilo mjini Katoro.

Na Mrisho Sadick:

Kanisa la EAGT Nazareth Stamico lililopo katika mji wa Katoro wilayani Geita limepanga kuanzisha ujenzi wa Hospitali ya kisasa katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuiunga mkono serikali katika jitihada za kusogeza huduma muhimu za afya karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza mara baada ya kupokea mkataba wa ununuzi wa kiwanja chenye thamani ya shilingi milioni 45 Mchungaji Tabitha January wa kanisa hilo amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni mwendelezo wa miradi ya kijamii inayotekelezwa na kanisa hilo kwa lengo la kuboresha ustawi wa jamii hasa katika sekta za afya na elimu.

Viongozi wa kanisa la EAGT wakipokea mkataba wa ununuzi wa kiwanja cha kanisa. Picha na Mrisho Sadick

Naye Katibu wa Kanisa la EAGT Nazareth Mussa Bernad amesema kanisa limekuwa likiendesha miradi mbalimbali ya kijamii kwa muda mrefu hivyo ujenzi wa hospitali hiyo ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma zinazotolewa na kanisa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ununuzi wa Kiwanja Gervas Daudi na Katibu wa Kamati hiyo Chacha Masiku wamesema mchakato wa ununuzi wa kiwanja hicho umefanyika kwa uwazi kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria na kanuni za kanisa, na kwamba hatua hiyo inatoa msingi thabiti wa kuanza rasmi maandalizi ya ujenzi.

Waumini wa kanisa la EAGT Nazareth wakiwa kwenye hafla ya mapokezi ya mkataba wa ununuzi wa kiwanja. Picha na Mrisho Sadick

Kupitia mradi huu Kanisa la EAGT Nazareth linatarajia kusaidia maelfu ya wananchi wa Katoro na maeneo ya jirani kupata huduma bora za afya, huku likidumisha ushirikiano wake na serikali katika kuimarisha ustawi wa jamii.

Sauti ya Ripoti kamili ya stori