Storm FM
Storm FM
15 October 2025, 3:07 pm

Ngombalemwiru ameeleza kuwa serikali atakayoiunda itaweka mfumo rafiki wa huduma za afya utakaolenga utu na heshima ya binadamu.
Na Mrisho Sadick:
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Wakulima Tanzania (AAFP) Kunje Ngombalemwiru ameahidi kuondoa kabisa ada zinazotozwa hospitalini kwa familia zinazochukua miili ya wapendwa wao waliopoteza maisha.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Karoro wilayani Geita Oktoba 14,2025 Ngombalemwiru amesema utaratibu huo umekuwa chanzo cha mateso kwa wananchi wengi hasa wa kipato cha chini wanaokabiliwa na gharama kubwa wakati wa majonzi.

Ngombalemwiru ameeleza kuwa serikali atakayoiunda itaweka mfumo rafiki wa huduma za afya utakaolenga utu na heshima ya binadamu akisisitiza kuwa hospitali hazipaswi kuwa chanzo cha mzigo kwa wananchi bali pa kutoa faraja na huduma bora.
Katika hatua nyingine mgombea Urais huyo amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, atatoa trekta kwa kila kaya 10 za wakulima ikiwa ni mkakati wa kukifanya kilimo kuwa chanzo kikuu cha uchumi wa taifa.
