Storm FM
Storm FM
11 October 2025, 6:37 pm

Ujio wa Dkt. Samia unaleta ari mpya ya kisiasa na ni fursa ya kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Na Mrisho Sadick:
Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Geita na Wananchi mkoani humo wamepanga kufanya mapokezi ya kihistoria kwa mgombea urais kupitia chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kuanza rasmi kampeni zake mkoani humo tarehe 12 na 13 Septemba mwaka huu.
Tangu kutangazwa kwa ratiba hiyo hamasa imekuwa kubwa kila kona ya mkoa wa Geita, wanachama wa CCM na wananchi wameahidi kukesha katika viwanja vya maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo Manispaa ya Geita wakisubiri kwa shauku ujio wa kiongozi huyo.

Akiwa katika viwanja hivyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa wanawake Tanzania UWT Mkoa wa Geita Lolensia Bukwimba na katibu wake Pili Lameck wamesema kuanzia leo Septemba 11 hadi 13 watakesha kwenye viwanja vya maonesho vya Dkt Samia Kuhakikisha wanamsubili Kiongozi huyo.

Maandalizi ya mapokezi hayo yamepamba moto yakihusisha shughuli mbalimbali za kijamii kama vile matembezi ya hamasa, usafi wa mazingira, wakizungumza baada ya shughuli hizo baadhi ya wanachama wamesema ujio wa Dkt. Samia unaleta ari mpya ya kisiasa na ni fursa ya kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Mgombea ubunge wa jimbo la Geita mjini Chacha Mwita Wambura amepongeza jitihada za wanachama wa UWT na wananchi kwa kuonyesha umoja na upendo mkubwa kwa chama, amesisitiza kuwa ujio wa Dkt. Samia utazidi kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali ya CCM na kuleta msukumo mpya katika utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho, hususan katika sekta za elimu, afya na miundombinu.
Dkt Samia Suluhu Hassan akiwasili mkoani Geita Septemba 12,2025 atapokelewa wilayani Mbogwe mkoani Geita , akiwa wilayani humo atafanya mkutano kisha kuelekea wilayani Bukombe, septemba 13 atafanya mkutano Geita mjini, Geita DC Katoro baadae kuhitimisha wilayani Chato.