Storm FM

Picha: Ajali yaua mmoja, kujeruhi wengine Geita

8 October 2025, 5:49 am

Muonekano wa mazingira ilipotokea ajali na kupelekea kifo cha mtu mmoja. Picha na mwandishi wetu

Licha ya elimu na jitihada mbalimbali zinazofanywa kuzuia ajali za barabarani, bado matukio ya ajali yamekuwa yakitokea na kupelekea vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.

Na: Mrisho Sadick

Mtu mmoja amefariki Dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia ajali ya gari aina ya Canter yenye namba za usajili T.573 DZW kugongana uso kwa uso na basi kampuni ya Mallesa’s Luxury lenye namba za usajili T.708 DPS katika kata ya Butengorumasa wilayani Chato mkoani Geita.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema ajali hiyo imetokea usiku wa Oktoba 07, 2025 wakati gari hilo la mizigo aina ya Canter likitokea Jijini Mwanza kwenda wilayani Kibondo mkoani Kigoma na basi likitokea Dar es salaam kwenda Geita mjini.

Baadhi ya mashuhuda na Askari wa polisi wakiwa eneo ilipotokea Ajali . Picha na mwandishi wetu

Taarifa za awali kutoka eneo la tukio zilieleza kuwa watu wawili wamefariki Dunia lakini taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Geita zimeeleza kuwa tukio hilo limetokea saa nane usiku, aliyefariki ni mtu mmoja ambae ni dereva wa gari la mizigo Said Ramadhani (23) mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma huku watu wengine wawili waliokuwa ndani ya gari hilo Ismail Omari (34) na Annastazia Yohana (25) wote wakazi wa Dar es Salaam wakipata majeraha na wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha Afya cha Katoro, abiria wengine wa basi wapo salama huku chanzo cha ajali hiyo kikielezwa ni uzembe wa dereva wa Canter kushindwa kuchukua tahadhali.

Ripoti ya mwandishi wetu Mrisho Sadick ikieleza zaidi
Hali ilivyokuwa baada ya ajali kutokea na kupelekea kifo cha mtu mmoja. Picha na mwandishi wetu