Storm FM
Storm FM
5 October 2025, 5:57 pm

Katika hali ya kusikitisha mwili wa mtoto Magreth Dickson (7) umekutwa umetelekezwa katika mtaa wa Katoma ikiwa ni siku sita tangu kutangazwa na kituo cha Storm FM kuwa amepotea.
Na: Ester Mabula
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 7 aitwae Magreth Dickson aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Kalangalala, amekutwa amefariki dunia ikiwa ni siku sita zimepita tangu aripotiwe kupotea nyumbani alikokuwa akiishi na bibi yake eneo la Katoma, kata ya Kalangalala manispaa ya Geita.
Bibi wa mtoto huyo maarufu kwa jina la mama Hawa ameeleza kuwa Jumatatu ya Septemba 29, 2025 mtoto huyo hakurudi nyumbani baada ya kumuaga kuwa anaenda kucheza na watoto wenzake kama ilivyo kawaida,baada ya kutoonekana bibi alitoa taarifa kwa uongozi wa mtaa na ndipo akaelekezwa kutoa taarifa Jeshi la polisi kwa hatua zaidi.

Baba na mama mzazi wa mtoto huyo wameeleza kusikitishwa na tukio la mtoto wao kukutwa amefariki na kuziomba mamlaka uchunguza undani zaidi ili kubaini wahusika wa tukio hilo
Akithibitisha taarifa za uchunguzi wa kitaalamu Daktari kutoka hospitali ya manispaa ya Geita Rashid Lugwisha ameeleza juu ya uchunguzi wa tukio hilo.

Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio kwaajili ya taratibu zaidi za kiuchunguzi ambapo walitoa ruhusa ya kuendelea na maziko kutokana na mwili wa marehemu kuharibika. Mwenyekiti wa mtaa huo Frank Elias Kwimania ameeleza juu ya hatua za maziko ya mwili wa marehemu.
