Storm FM

PM Majaliwa atoa maagizo walimu kurundikana mijini Geita

3 October 2025, 5:35 pm

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye maadhimisho ya siku mwalimu Bukombe. Picha na Mrisho Sadick

Mhe Majaliwa akiwa Bukombe amesema hakuna sababu ya walimu kurundikana mijini wakati vijijini kuna uhitaji mkubwa .

Na Mrisho Sadick:

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais utumishi wa umma kuhakikisha wanaweka usawa wa walimu katika maeneo ya vijijini na mijini, kwakuwa idadi kubwa ya walimu wanakimbilia mijini hali inayosababisha upungufu mkubwa kwenye shule za vijijini.

Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika wilayani Bukombe mkoani Geita, ambapo amesema serikali inaendelea kuboresha makazi ya walimu pamoja na kuongeza walimu kutoka elfu 11 hadi elfu 13 mkoani Geita, huku zaidi ya walimu 7,500 wakipandishwa madaraja nakwamba hakuna sababu ya walimu kurundikana mijini ili hali vijijini kuna uhitaji mkubwa.

Naibu Waziri Mkuu Dkt Biteko akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mwalimu. Picha na Mrisho Sadick

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema serikali itaendelea kusimama na walimu katika kuimarisha sekta ya elimu, huku akiitaka jamii kuwathamini walimu kwakuwa wao ndio nguzo ya maendeleo ya Taifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Carolyne Nombo amesema wizara imeweka mikakati ya kutoa mafunzo endelevu na kuhakikisha mazingira ya kazi ya walimu yanaimarika ili kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Walimu kutoka maeneo mbalimbali mkoani Geita wakiwa kwenye maadhimisho ya siku mwalimu duniani wilayani Bukombe. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema mkoa huo bado unakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu, hususan maeneo ya vijijini, na kuahidi kushirikiana na wizara ili kuhakikisha kila shule inapata walimu wa kutosha.

Viongozi mbalimbali wakiwa katika maadhimisho ya siku ya mwalimu duniani wilayani Bukombe. Picha na Mrisho Sadick

Awali Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Geita Pauline Ntinda akiwasilisha taarifa ya chama hicho, ameiomba serikali kuongeza kasi ya kuboresha maslahi ya walimu na kuhakikisha changamoto za makazi na vifaa vya kufundishia zinapatiwa ufumbuzi huku akipongeza juhudi za serikali kuendelea kupandisha walimu madaraja.

Sauti ya ripoti kamili ya stori hii