Storm FM
Storm FM
2 October 2025, 3:52 pm

TAKUKURU imeendelea na mikakati mbalimbali ya kutoa elimu kwa UMMA ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 kwa lengo la kuhakikisha mazingira huru, haki na yenye uwazi.
Na: Ester Mabula
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Geita leo Oktoba 02, 2025 imekutana na viongozi wa dini kwa lengo la kutoa elimu juu ya mapambano dhidi ya rushwa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Elimu hiyo imetolewa katika ofisi za TAKUKURU zilizopo kata ya Kalangalala manispaa ya Geita, akizungumza awali kabla ya elimu kutolewa, Naibu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Geita Alex Mpemba amesema viongozi wa dini ni kiungo muhimu kati ya taasisi na jamii, na hivyo wana nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa na namna ya kuripoti vitendo hivyo.

Wakizungumza Askofu Stephano Saguda mwenyekiti mwenza wa dini mbalimbali mkoa wa Geita na Kadhi wa mkoa wa Geita Sheikh Ibnubazi Rajabu wamesisitiza kuwa watatumia nafasi zao kuelimisha waumini kupinga vitendo vya Rushwa ili kuwa na Jamii yenye haki na Taifa lenye maendeleo na usawa

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria kikao hicho wameipongeza TAKUKURU kwa hatua hiyo na kuiomba iendelee kuelimisha Jamii kupitia mikutano ya hadhara, kuwafikia wanafunzi mashuleni sambamba na utoaji wa vipeperushi ambavyo vitasaidia kusambaza elimu kwa ukubwa zaidi
