Storm FM
Storm FM
29 September 2025, 1:20 pm

Kupitia risala yao wanafunzi wa shule ya sekondari msalala wameishukuru serikali kwa uwekezaji huo na kuiomba kuwasaidia kupata basi la shule
Na Mrisho Sadick:
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msalala wilayani Nyang’hwale mkoani Geita pamoja na wananchi wa eneo hilo wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa ukumbi wa kisasa, mabweni na maboresho makubwa ya miundombinu shuleni hapo.
Katika Mahafali ya 27 ya Kidato cha Nne yaliyohusisha wahitimu 254 wanafunzi wamesema maboresho yaliyofanyika yameleta mapinduzi makubwa ya kielimu kwa kuwapatia mazingira bora ya kujifunzia na kuishi shuleni huku kupitia risala yao wameishukuru serikali kwa uwekezaji huo na kuiomba kuwasaidia kupata basi la shule litakalorahisisha usafiri wa pamoja.

Wazazi na wananchi wa Nyang’hwale nao wameeleza kufurahishwa na jitihada hizo wakisema kuwa uwekezaji wa elimu umekuwa kichocheo cha hamasa ya wanafunzi pamoja na ufaulu unaoongezeka mwaka hadi mwaka huku wakiwataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kupata ufaulu mzuri zaidi.
Afisa Elimu sekondari wa Wilaya hiyo Linus Anatory amesema kuwa uwekezaji katika miundombinu ya shule umekuwa chachu ya kuongezeka kwa ufaulu ambapo mwaka jana ufaulu ulikuwa asilimia 92 na mwaka huu wamepanga kufikia asilimia 100 kutokana na mikakati madhubuti ambayo wamejiwekea.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Nyang’hwale, Abdala Mohamed, aliahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ili kuhakikisha changamoto ya basi la shule inapatiwa ufumbuzi wa haraka.