Storm FM
Storm FM
10 September 2025, 4:17 am

Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wameendelea kuzungumza na wananchi kunadi sera za ilani ya vyama vyao ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kwenye Uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Na: Ester Mabula
Baadhi ya Wananchi wa mtaa wa Mwatulole na Nshinde Kata ya Buhalahala Jimbo la Geita Mjini wamemuomba Mgombea Ubunge kwa Tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo hilo, Mhandisi Chacha Mwita Wambura, kuwatatulia changamoto ya maeneo ya malisho ya mifugo endapo atapata ridhaa ya kuwaongoza.
Wakizungumza Septemba 09, 2025 mara baada ya mgombea huyo kuwatembelea katika maeneo yao ya biashara kujitambulisha, wametumia nafasi hiyo kumuomba mgombea huyo iwapo atapata nafasi ya kuliongoza jimbo hilo kuwekeza nguvu kubwa katika kushughulikia kero ya miundombinu ya barabara ambazo zimekuwa tatizo la muda mrefu.

Awali akizungumza na wananchi hao mhandisi Chacha amesema kupitia kauli mbiu yake ya “Geita Mpya, Kazi na Matokeo” wananchi watarajie matokeo chanya katika miaka atakayowatumikia.
Akiwa katika soko la Mwatulole lililopo kata ya Buhalahala, wafanyabiashara na wajasiriamali katika soko hilo wameomba kuboreshewa miundombinu ya soko kwani soko hilo halina choo hali ambayo inapelekea ugumu kwenye ufanyaji wa biashara

Mhandisi Chacha Wambura, amesema iwapo watampa ridhaa ya kuwaongoza, atashughulikia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao ikiwemo uboreshaji wa maeneo yao ya kufanyia biashara na kuhakikisha wanapata mikopo yenye masharti nafuu pamoja na elimu ya matumizi bora ya mikopo inayotolewa na Halmashauri.
